HALMASHAURI YA WILAYA YA MEATU
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA TASAF AWAMU YA TATU
Mpango wa TASAF wa Kunusuru Kaya Maskini
1.0 Utangulizi
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini chini ya TASAF awamu ya III ulianza katika Halmashauri ya Meatu tarehe 17/07/2014 kwa kujenga uelewa wadau mbalimbali juu ya Mpango huo. Zoezi la kutambua kaya maskini liliendeshwa kuanzia tarehe 21/07/2014 hadi 10/09/2014 katika vijiji 64 vilivyoteuliwa kushiriki katika mpango huu ambapo kaya maskini 7,020 zilitambuliwa. Zoezi hilo lilifuatiwa na zoezi la kuhakiki na kuandikisha kaya hizo kuanzia tarehe 13/10/2014 hadi 16/11/2014 ambapo kaya 5,810 ziliandikishwa. Hatimaye kaya 5,800 ziliidhinishwa na TASAF makao makuu kwa ajili ya kupokea malipo ambayo yamekuwa yakifanywa kwa vipindi vya miezi miwili miwili kuanzia Julai 2015.
2.0 Idadi ya walengwa walionufaika na wasionufaika
Malipo ya walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini yamefanyika kwa vipindi vitano tofauti ambapo jumla ya shilingi 1,040,409,174/= zimelipwa. Vipindi hivyo vya malipo ni Julai & Agosti 2015, Septemba & Oktoba 2015, Novemba & Desemba 2015, Januari & Februari 2016, na Machi & Aprili 2016 .
Jedwali hapa chini linaonesha idadi ya kaya zilizoizinishwa, zinazonufaika na zisizonufaika katika vipindi vyote vya malipo
KIPINDI CHA MALIPO |
IDADI YA KAYA ZILIZIIDHINISHWA |
IDADI YA KAYA ZILIZOLIPWA |
IDADI YA KAYA AMBAZO HAZIKULIPWA |
Julai & Agosti 2015
|
5,800 |
5,634 |
166 |
Septemba & Oktoba 2015
|
5,800 |
5,702 |
98 |
Novemba & Desemba 2015
|
5,800 |
5,636 |
161 |
Januari & Februari 2016
|
5,800 |
5,700 |
100 |
Machi & Aprili 2016
|
5,800 |
5,479 |
321 |
2.1 Sababu za baadhi walengwa kutolipwa:
- Kutojitokeza kwa walengwa na kushindwa kutuma wawakilishi kwa ajili ya kuwapokelea fedha zao siku za malipo.
- Kufariki dunia kwa mlengwa asiye na mtegemezi.
- Kusimamishwa kwa malipo baada ya mlengwa kutambuliwa na mkutano maalum wa kijiji mwezi Februari 2016 kuwa hana sifa za kuwa mlengwa wa Mpango.
3.0 Manufaa ya Malipo kwa Walengwa
- Kaya maskini zimenufaika na malipo yanayotolewa na Mpango na zimeweza kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha hali ya maisha yao ikiwemo haya yafuatayo:
- Kutosheleza mahitaji ya shule kwa watoto kama kununua sare za shule, vitabu, daftari na kalamu.
- Kuimarisha afya ya familia kwa kulipia gharama za matibabukujiunga na Mfuko wa afya ya jamii (CHF).
- Kuboresha makazi ya familia kwa kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba kama vile mabati, misumari na saruji.
- Kuanzisha miradi midogo midogo ya ujasiriamali kama vile ufugaji wa mbuzi na kuku wa kienyeji kwa ajili ya kuboresha lishe na kuinua kipato cha familia.
- Kununua mahitaji ya familia kama vile mavazi, sabuni na chakula (mfano, sukari, majani ya chai, chumvi, mafuta ya kupikia na nyama).
4.0 Changamoto
- Baadhi ya majina ya watoto wanaotakiwa kutimiza masharti ya elimu na afya yanayotumwa Halmashauri kutoka TASAF makao makuu kwa ajili ya kuhakiki mahudhurio kugundulika kuwa sio majina ya watoto wa shule au vituo vya afya wanakotakiwa kuhudhuria. Taarifa hizi zimefikishwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho.
- Kaya nyingi zilizotajwa katika mikutano ya vijiji ya kubaini kaya zisizo na sifa iliyofanyika Februari 2016 kujitokeza kwa ajili ya malipo na kuonyesha kutokubaliana na maamuzi ya mikutano hiyo ya vijiji. Kaya hizo zitatembelewa kwa ajili ya uhakiki.
- Idadi ya kaya zinazoishi katika lindi la umaskini katika Halmashauri ya Meatu bado ni kubwa. Kaya hizi zipo katika vijiji vinavyohudumiwa na Mpango na pia katika vijiji ambavyo bado havijafikiwa na Mpango. Orodha ya vijiji ambavyo bado havijafikiwa na Mpango ilitumwa TASAF makao mwaka 2015.
5.0 Hitimisho
Utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini unaendelea vizuri katika Halmashauri ya Meatu. Jumla ya shilingi 1,040,409,174 zimelipwa kwa walengwa na wameweza kunufaika kwa kiasi kikubwa.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.